Mabao mawili ya winga mtokea benchini Mrisho Ngasa yaliirejesha
Yanga kileleni mwa msimamo wa VPL juzi baada ya kuilaza Mtibwa Sugar 2-0
kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Jemedari Said, meneja wa timu ya Azam, alisema jana
kuwa Yanga wana muda wa siku tatu (saa 72) tu za kukaa kileleni mwa
msimamo wa ligi hiyo kwani anaamini kikosi chake kitafanya kweli katika
mechi yao ya mkononi kesho dhidi ya Mtibwa na kurejea kwenye nafasi
hiyo.
"Tuliteleza Morogoro Jumamosi na kujikuta tukilazimishwa sare dhidi
ya Polisi Moro. Jumatano (kesho) tutakuwa na mechi ya kiporo dhidi ya
Mtibwa Sugar. Ingawa tunakutana na timu yenye ushindani wa kweli msimu
huu, ninaamini tutashinda na kurejea katika nafasi yetu," alisema
Jemedari.
Azam FC iliiondoa Yanga kileleni baada ya kuambulia sare ya 2-2
dhidi ya Polisi Moro mjini Morogoro Jumamosi ikifikisha pointi 22,
lakini ushindi wa juzi dhidi ya Mtibwa Sugar uliifanya Yanga kufikisha
pointi 25 na kurejea kushika usukani.
Mtibwa inayonolewa na nahodha wake wa zamani, Mecky Mexime, imekuwa
haipati matokeo mazuri inapocheza dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa
Azam, Dar es Salaam.
Hata hivyo, Mexime amewataka wachezaji wake kutokata tamaa kutokana
na kipigo cha juzi dhidi ya mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, bali
wageuzie akili zao katika mechi ya kesho dhidi ya Azam.
CHANZO:
NIPASHE






0 comments:
Post a Comment