Mbeya/Dar. Ni urafiki wenye shaka. Hivyo, ndivyo unavyoweza kuzungumzia hatua ya mashabiki wa Prisons na Mbeya City kuungana ili kuimaliza Yanga.
Katika kikao cha pamoja, mashabiki hao wa klabu hizo kubwa mbili za Mbeya walikubaliana kuunganisha nguvu, kuzishangalia timu zao kwa pamoja dhidi ya Yanga.
Makubaliano hayo yamefikiwa wakati Jiji la Mbeya likianza kindumbwendumbwe cha timu zake kuikabili Yanga ya Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Sokoine.
Kikao hicho kilichofanyika viwanja vya City Pub, mashabiki hao walikubaliana kuwa kuanzia leo watakuwa kitu kimoja ili kuishangilia moja ya timu hizo itakapocheza na timu ngeni jijini humo.
Hata hivyo, wamesisitiza kwamba timu hizo zikikutana kwenye mechi za ligi au kirafiki, mashabiki wao wataendeleza utani wa jadi kwa kila kundi kuishangilia timu yao.
Msemaji wa Mbeya City, Dismas Ten alisema mashabiki hao walikutana na kuanzisha sura mpya ya kuzishangilia timu zao na kwamba kwa kuanzia itakuwa mechi ya leo ya Prisons dhidi ya Yanga.
Shabiki wa Prisons, Tawi la Iyunga, Aden Kinyuke alisema hatua ya kuungana kwa mashabiki hao ni kuutakia mema mkoa wao ili uweze kubaki na timu mbili Ligi Kuu. Kuhusu mechi hiyo, Kinyuke alisema Prisons imejipanga kwa hali na mali kuitandika Yanga.
Tayari, Yanga imetangaza azma ya kunyakua pointi sita mkoani Mbeya kutoka kwa Prisons leo na Mbeya City, Jumapili.
Kocha Hans Pluijm alisema juzi kwamba wapo Mbeya kupata pointi na siyo kutalii na kwamba hayo ndiyo malengo yao.
Yanga, Azam zasaka pointi ugenini
Ukiacha ushabiki huo wa Mbeya, Yanga na Azam baada ya mechi zao za kimataifa, mwishoni mwa wiki zinataka kufanya vizuri kwenye ligi ambako zinakimbizana. Leo, zitakuwa ugenini kwenye michezo yao dhidi ya Prisons kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya na Mabatini, Mlandizi, mkoani Pwani ambako Azam itacheza na Ruvu Shooting.
Azam iliifunga mabao 2-0 El- Merreikh ya Sudan kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Yanga kupata ushindi kama huo, dhidi ya BDF XI ya Botswana kwenye Kombe la Shirikisho.
zaidi>>mwananchi






0 comments:
Post a Comment